Tuesday, May 17, 2016

Ilipoishia ya jana

MAUMIVU ya mapenzi yamemfika shingoni Millar Foster, sasa ameamua kumfuata mpenzi wake nchini Afrima. Kwa siku tatu ambazo Mika ameondoka Marekani, Millar amekonda, maumivu ya mapenzi hayaelezeki analia sana maana mpenzi wake amekwenda nchi yenye vita. lakini sasa ameamua kupanga kumfuata.

Mika yuko nchini Kenya sasa anasubiri basi la kuelekea mji wa Kakma kuliko kambi ya wakimbizi ambayo anahisi huenda akamuona mama na mdogo wake.

Kamanda Alfatt anawaadhibu wanajeshi wake viboko 100, ili aonekane mtu safi machoni pa mtu ampendaye Leah binti wa Isabella.

SASA ENDELEA

Wakati adhabu hiyo ikiendelea kwa mbali kamanda Alfatt alikuwa akimtazama Leah msichana mpole na mzuri ajabu moyo wake ukikimbia mbio za mita 100 kwa sekunde tano.

Kwa kutoa adhabu ile, tena mbele ya watu, kamanda Alfatt alijua wazi kuwa msichana Leah atalidhika na atamuona kuwa ni mtu anayefaa katika jamii ya wakimbizi, hiyo itakuwa moja wapo ya njia ya kumpata Leah msichana wa ndoto ya maisha yake.

Aliyakumbuka maneno ya Leah aliyoambiwa siku ile Leah alipokuja kulalamika mbele yake juu ya kubakwa kwa rafiki yake Ashina kuwa yeye kama kamanda na kiongozi wa kambi, kwa nini anaacha matendo kama hayo yatendeke pale Monja.

Ilikuwa ni adhabu kali kwa wale wanajeshi wawili waliombaka msichana Ashina, eneo lile lote walilopatiwa adhabu lilikuwa limetapakaa damu, wote walikuwa wamezimia maana viboko vilikuwa vimewachanja mwili mzima.

Baada ya viboko 100 kukamilika walifunguliwa kwenye ile miti ya adhabu na kupelekwa sero.

Kamanda Alfatt akijua tayari kazi ya kujitetea mbele ya Leah na Isabella imekwisha, alishuka jukwani na kuelekea ofisini kwake, huku nyuma akiwaacha wote katika maswali. Maana kiukweli kamanda Alfatt alikuwa amebadilika.

Kamanda wa kike aliamuru wakimbizi wote warudi kwenye makazi yao. Watu waligeuka na kurudi kwenye vibanda vyao. Huko vibandani waliendelea kujiuliza inakuwaje kamanda aliyekuwa mkatili na muuaji dhidi yao, leo amegeuka na kuwa mtu mwema anayewatetea, hawakujua kamwe.

Lakini Leah alikuwa akiongea na mama yake wakiwa kibandani kwao kuhusu kaamanda wa Alfatt.

      “Mama unasikia watu wanavyosema, juu ya kamanda mkuu wa kambi?” aliuliza Leah.

      “Nasikia watu wanasema kamanda Alfatt kabadilika hakuwa mtu wa kuwatetea, hawaamini kwa yeye leo kutoa adhabu kwa wanajeshi wake waliobaka,” alijibu Isabella.

Mama Ashina aliyekuwa anamnywesha mwanaye Ashina uji alidakia yale maongezi.

     “Ni kweli lazima itushangaze kwa kuwa matendo maovu yametendeka hapa Monja kwa muda mrefu, lakini haikuwahi kutokea wanajeshi wake wanaofanya uovu huo, yeye kuwaadhibu, leo ni jambo la ajabu sana,” aliongea Melina mama Ashina kwa majonzi ambaye naye alishawahi kubakwa.

     “Nadhani kuna kitu anatafuta, kama sio anampenda mwanangu?” aliongea Isabella akimtazama mwanaye Leah.

Leah naye akamjibu mama yake..

    “Hata mimi nahisi ananipenda kwa kuwa baada ya mimi kwenda kulalamika na kulia mbele zake alionyesha sura ya huruma na ikampelekea kutoa adhabu hii.”

     “Hata mimi nahisi anakupenda, kwa nini nasema hivyo, kwa sababu maovu yote yaliyokuwa yanatendeka hapa, watu walikuwa wanakwenda kushtaki kwake lakini hakuwa akichukua hatua yoyote zaidi aliwapiga na kuwafukuza wale waliokuwa wanakwenda kushtaki,” aliongea Melina akiwa amemlaza mwanaye Ashina kwenye mapaja yake.

     “Mwanangu amembadilisha kamanda huyu lakini je moyo wake wa ukatili bado anao?”

 Isabella alimsogelea mwanaye akamtazama kwa huruma akamshika kichwani kwa mikono yake miwili akamwambia..

     “Mwanangu! Sipendi uwe karibu na kamanda huyu lakini kwa ajili ya hawa wakimbizi wenzetu inakubidi uwe karibu naye.”

     “Mamaa!” aliongea Leah kwa mstuko kidogo asimuelewe mama yake.

    “Ni kweli! Nisikilize mwanangu, wewe ni shujaa pekee kati yetu sisi wakimbizi, unaweza ukabadili taswira nzima ya maisha ya watu hapa Monja. Umesikia mwenyewe kuwa kabla ya sisi hatujaletwa hapa, maovu yaote yalikuwa yanatendeka bila kujali watu hawa ni binadamu na raia wa taifa hili. Lakini tulipokuja sisi maisha yameanza kubadilika. Unakumbuka siku tatu zilizopita kamanda mkuu aliwasamehe wale watu waliotaka kutoloka hapa kambini wasiuawe? Leo amewaadhibu wanajeshi wake hauoni hilo ni jambo zuri kwa upande wetu na hii yote kwa sababu anakupenda wewe. Sasa nachokuomba mwanangu jitahidi kuwa karibu naye ujifanye kama unamuelewa na akikutamkia anakupenda usimkubalie ila onyesha kama utamkubalia kesho na kesho kutwa ili ajue kuwa anachokifanya kwa sasa wewe unakikubali. Hii itakuwa salama kwetu sisi na watoto wetu utakuwa umewaokoa watu wengi sana mwanangu, kamanda huyu roho yake imeshabadilika kwa kuwa amekuona wewe, na endapo hatakuona mbele yake moyo wake wa ukatili utamrudia tena. Hatuna njia nyingine y
a kujiokoa ila ni wewe mwanangu waokoe watu wa taifa lao ambao walishakosa matumaini na jeshi la serikali yao sawa mwanangu,” aliongea Isabella kwa msisitizo akimtazama mwanaye Leah ambaye alionyesha ujasiri na kuukubali ushauli wa mama yake.

No comments:
Andika comments

Shukrani

Aina za Habari

Hifadhi