Friday, May 13, 2016

Polisi wageuza sukari dili

WAFANYABIASHARA Jijini Dar es Salaam wamelalamikia baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kuwanyanyasa kwa kisingizio cha kutafuta sukari iliyofichwa.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, wamiliki wa maduka ya jumla yaliyopo Kitumbini Manispaa ya Ilala walisema wameanza kupata usumbufu huo kutoka kwa askari hao tangu kuanza kwa msako wa sukari inayodaiwa kufichwa na wafanyabiashara.

Mfanyabiashara Albert Ndembuka, alisema hivi karibuni alivamiwa na askari wanne ambao  walimfanyia upekuzi kwa madai kuwa ameficha sukari.

“Vyombo vya usalama wamefanya tatizo hili ni fursa kwao kujipatia fedha haramu,” alisema Ndembuka na kuongeza:

“Sifanyi kazi kwa raha kwa sababu ya usumbufu mkubwa ninaopata kutoka kwa askari ambao wamekuwa wakinivamia hadi nyumbani kutaka kunipekua kwa sababu ya kuuza sukari.

Mfanyabiashara Mtaa wa Agry Kisutu, Geofrey Peter Aggrey alisema askari wanawasababishia usumbufu mkubwa kwa kukamata sukari wakati wakiisafirisha kutoka kwenye maghala kwa madai ya kuikagua.

“Usumbufu ni mkubwa, kuna watu juzi walikamatwa wakiwa wametoka kununua sukari wakiwa na vibali vyao mkononi lakini askari hao walidai lazima wakaguliwe kwanza hivyo mtu anaona kuliko aendelee kusumbuliwa bora awape fedha wamwache aendelee na biashara yake,” alisema Peter.

Kuhusu upatikanaji wa sukari, Peter alisema kuna usumbufu mkubwa wa kupata bidhaa hiyo na kuifanya iendelee kuuzwa bei ya juu kuliko ile iliyoelekezwa na serikali.

“Tunapanga foleni kuanzia asubuhi hadi jioni kutafuta kibali na hatimaye usipate sukari, inabidi tutumie madalali ambao nao wanaongeza gharama ya sukari.

Alisema kutokana na usumbufu huo hadi kuifikisha dukani mfuko wa kilo 20 unagharimu Sh 39,000 hadi 40,000 badala ya Sh 35,000 ya awali.

“Agizo la serikali haliwezi kutekelezeka kwa sababu hadi kufika kwa walaji inapaswa kuuzwa kwa Sh 1,800, lakini bei hiyo ndiyo tunayouziwa na wakala hivyo lazima tutauza Sh 2,000 na hadi kumfikia mlaji bei itakuwa kati ya Sh 2,100 na 2600,” alisema Peter.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kinachofanywa na polisi ni kuhimiza wafanyabiashara kutoficha sukari kwani ni makosa kisheria.

Alisema ukaguzi unaofanywa na askari polisi ni wa kawaida pale anapotilia shaka na unafanywa kwa  nia njema ambapo aliwataka wananchi kutoa taarifa kama kuna askari atakaye onyesha nia mbaya ya kutaka kupewa rushwa.

“Askari wanafanya ukaguzi kwa nia njema pale wanapotilia shaka na akimaliza uchunguzi wake kama hakuna ukiukwaji wa taratibu huyo mtu anaachiwa lakini kama wapo askari wenye nia mbaya tunaomba wananchi watoe taarifa.” alisema Senso.

Wakati huo huo mmiliki wa Kampuni ya Tanzania Commodities Trading Group, Murtaza Dewji amekana kuficha sukari tani 2,990 zilizokutwa Bandari Kavu (ICD) ya PMM iliyopo Vingunguti, jijini Dar es Salaam.

Sukari hiyo ambayo ilihusishwa moja kwa  moja na Kampuni ya Mohamed Enterprises, ilidaiwa kukamatwa juzi katika msako maalum ulioendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Poul Makonda.

Akizungumzia hatua hiyo, Dewji alikanusha kampuni yake kuwa na uhusiano na Metl, lakini pia alisema kuwa hajawahi kuficha sukari na kwamba sukari yake iko kihalali na inavyo vibali vyote stahiki.

No comments:
Andika comments

Shukrani

Aina za Habari

Hifadhi