Saturday, April 30, 2016

Sara: Kifungo kimenipa mtoto

lakini pia kutoa mafunzo kwa wanariadha wachanga
NYOTA wa mchezo wa riadha nchini, Sara Ramadhani, amesema adhabu ya kufungiwa miaka miwili aliyopewa na Shirikisho la Riadha la Dunia (IAAF), imeweza kumpa faida ya kupata mtoto na kuibua vipaji vya wanariadha wapya katika jamii inayomzunguka.

IAAF ilimfungia Sara baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kutumia dawa za kusisimua misuli.

Sara ameliambia Dimba kuwa katika kipindi alichokuwa akitumikia adhabu hiyo, ameweza kupata mtoto wa kike ambaye kwa sasa ana mwaka mmoja lakini pia kutoa mafunzo kwa wanariadha wachanga watano ambao wameshaanza kushiriki mashindano ya ndani mkoani Arusha.

Alisema licha ya kuumizwa na adhabu hiyo lakini anajivunia faida aliyopata, ambayo kama si kufungiwa pengine asingepata fursa ya kupata mtoto na kushiriki kwenye kuibua vipaji.

“Kila jambo lina sababu zake na Mungu ndiye mpangaji wa kila jambo, sitoweza kumlaumu mtu kwa lililotokea hapo awali lakini pia nashukuru Mungu kupitia mtihani wa kufungiwa nimeweza kuongeza familia kwani atakua mtoto wangu wa pili."

"Pia najivunia kuibua wanariadha chipukizi watano ambao nawapa mafunzo ya mchezo wa riadha kwa kushirikiana na mume wangu ambaye ndiye kocha wangu pia,” alisema.

Sara alikutwa na kosa la kutumia dawa za kuongeza nguvu wakati alipokuwa akishiriki michuano ya mwaliko wa kimataifa mwaka 2014 nchini Brazil.

No comments:
Andika comments

Shukrani

Aina za Habari

Hifadhi