Thursday, June 2, 2016

Magonjwa ya kuku

Katika makala za mwanzo tuliona kuhusu ugonjwa wa Newcastle ama  Kideli kama ulivyoeleka. Na kitaalam ugonjwa huu hujulikana kama sotoka ya kuku.. huwa ipo sotoka ya ng'ombe.
Ni muhimu mfugaji ukawa na elimu kuhusu magonjwa haya maana kuku kama walivyo wanyama wengine hupatwa na magonjwa mbalimbali ambayo kwako ni changamoto kubwa katika biashara yako

Dondoo Muhimu:
Inampasa Mfugaji kuzuia magonjwa kabla ahayajashambulia kuku wake kwa kuzingatia kwamba siku zote kinga ni bora kuliko tiba.
*Hakikisha kuku wako unawalisha chakula bora. Na kwa kiwango kinachotakiwa.
*Mazingira lilipo banda la kuku na banda lenyewe yawe safi.
*Vyombo vya kunyweshea maji kuku na vile vya chakula viwe safi.
*Usafi wa nyumba ya kuku ni muhimu sana.
*Nyunyuzia dawa ya kuzuia wadudu katika kuta na milango.
*Weka dawa mlangoni ya kuzuia wadudu ambayo kila aingiaye kwenye Banda la kuku advantage hapo kabla ya kuingia bandani.
*Hakikisha unadhibiti idadi ya watu wanaoingia kwenye Banda la kuku wako kuepusha magonjwa kwa Sababu wanaweza kuwa wamebeba magonjwa kutoka huko walikotoka.

NDUI YA KUKU (Fowl Pox).
DALILI ZAKE:
Kuku huonekana na vipele vya rangi ya kijivujivu, kwenye ngozi yake, hasa kwenye upanga wa kichwa. Baada ya muda mfupi vipele hivi huwa vikubwa na kukutana na kufanya majeraha mabichi na yenye kutoa damu.
Baada ya siku kumi hadi kumi na nne hivi, majeraha haya hukauka na kufanya makovu meusi. Kuku wanaougua wanaweza kutibiwa lakini mfugaji inampasa atoe taarifa haraka kwa daktari wa mifugo aliye karibu naye ili ampatie dawa zinazofaa.
Kuku wanaougua watengwe haraka wanapoonekana ili wasiambukize wazima. Usafi ni muhimu katika kuzuia ugonjwa huu usitokee. Kuku wapewe nafasi ya kutosha na wasisongamane.
Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kabisa kwa kuchanja chanjo ya Fowl Pox. Chanjo hii huchanjwa kuku katika Mbawa zao.

KIPINDUPINDU CHA KUKU(Fowl Cholera)
Ugonjwa huu unapomjia kuku kwa nguvu, hufa ghafla. Unapomjia taratibu kuku husinzia na manyoya yake huvurugika. Shingo huinamia nyuma. Upanga na ndevu hupanuka. Kuku huishiwa hamu ya kula chakula, na kuharisha kinyesi cheupe. Baadhi ya kuku huvuta pumzi kwa shida na kutoa sauti ya mkwaruzo. Mfugaji amwarifu daktari wa mifugo aliye karibu naye, na atamshauri dawa za kutumia. Usafi wa nyumba na uwanya wa kuku ndiyo msingi wa kuzuia ugonjwa huu. Kuku walioshikwa na ugonjwa huu watengwe haraka na baadaye wachomwe moto. Kuku wachanjwe dawa mapema kwenye sehemu ambazo ugonjwa huu hutokea mara kwa mara.

HOMA YA MATUMBO KWA KUKU(Fowl Typhoid)
Kuku anapopata ugonjwa huu kwa nguvu sana upanga na ndevu zake hukunjamana. Kuku hufa ghafla japokuwa huonekana bado ana afya sana. Ikiwa ugonjwa unamjia kwa taratibu hadi ukakomaa, upanga na ndevu hufifia na kunyauka. Kuku huhara kinyesi cha rangi ya manjano. Hamu ya chakula humtoka, isipokuwa hunywa maji mengi, na kuku huyo huonekana ana wasiwasi sana. Kuna dawa nyingi ambazo zinaweza kusaidia kuponya baadhi ya kuku wakati ugonjwa huu unapoingia. Dawa hizi mara nyingi hutengenezwa ili zitumiwe kwenye chakula au maji. Mfugaji amwone daktari wa mifugo aliye karibu naye ili amshauri dawa ya kutumia. Nyumba za kuku ziwekwe kwenye hali ya usafi, na uwanja usafishwe pia. Vyombo vya maji na chakula visafishwe kwa dawa. Kuku wanaougua wote wachomwe moto. Kuku wazima wachanjwe dawa mapema na ikiwezekana wachunguzwe kila mmoja kuona kama wapo wenye ugonjwa huo.

WADUDU WANAOKAA KWENYE MANYOYA YA KUKU.
Mfugaji inampasa awachunguze kuku wake mara kwa mara, ili ahakikishe kuwa kuku wake hawana viroboto, chawa, papasi au wadudu wengine ambao ni wadogo sana hata ni vigumu kuwaona kwa urahisi kwa macho. Wadudu hawa huwasumbua kuku na kuwapunguzia uwezo wao wa kutoa mazao mengi ya mayai au nyama. Ni jambo la busara kutumia dawa za wadudu ambazo hutengenezwa katika hali ya unga. Dawa hizi hutumika kwa kuwapaka kuku au kumwagia sakafu, au kwenye masanduku ya kutagia, au kwenye ngazi za kupumzika kuku. Mfugaji amwone daktari wa mifugo aliye karibu naye ili amshauri dawa zinazofaa kwa sehemu yake. Kuna baadhi ya wadudu wa kuku ambao wanakaa kwenye miguu ya kuku na kufanya magamba miguuni. Mfugaji anaweza kutumia mafuta ya taa kwa kupaka miguu mpaka atakapoona kuwa wadudu wote wametoweka.

UGONJWA WA MINYOO
Kuku hushambuliwa na aina nyingi za minyoo ambayo huishi tumboni na kuwanyonya damu au chakula na kuwadhoofisha, au kuwauwa kabisa. Njia iliyo bora ya kuzuia minyoo hii ni usafi wa nyumba na uwanja wa kuku. Hali ya kuambukiza ya minyoo ikizidi, mfugaji amwarifu afisa mifugo aliye karibu naye, ili amshauri dawa za kutumia.

KUDONOANA MANYOYA, VIDOLE, KUUMIZANA AU KUPIGANA WENYEWE NA KULA MAYAI.
Tabia hizi mbaya za kuku hutokana na sababu nyingi mbalimbali. Sababu mojawapo ni upungufu wa nafasi ambayo hufanya kuku wasongamane sana. Kwa hiyo kuku wapewe nafasi ya kutosha ya chakula maji na ya kupumzika. Kuku wanaweza kuanzisha tabia hizi ikiwa chakula chao hakina aina zote za chakula hasa nyama au chumvi au vitamini. Kwa hiyo njia mojawapo ya kuepukana na tabia hizi mbaya ni kuwapa kuku chakula bora. Wakati mwingine kuku hushawishiwa kula mayai kutokana ukosefu wa kuondoa mayai kwenye nyumba ya kutagia, mara kwa mara. Kwa hiyo mayai ni lazima yaondolewe kwenye nyumba za kutagia mara tatu au zaidi kwa siku.

Uchovu wa kukaa mahali pamoja unaweza kuwafanya kuku waanze baadhi ya tabia hizi mbaya. Wafugaji wengi wenye busara huwazuia kuku wasianze tabia hizi kwa kuwapatia majani mabichi ambayo huwafanya wawe na mchezo wa kupoteza na kusahau kudonoana. Majani hayo hutundikwa kwa kamba. Njia nyingine ambazo hutumika kwa kuzuia tabia hizi mbaya za kuku ni kuwakata midomo kwa kutumia kisu kilichopashwa moto, au chuma cha moto wanachotumia mafundi kuungia. Ubora wa chombo kilichopashwa moto ni kwamba mdomo wa kuku hukatwa na kuzuia damu isitoke. Kwa hiyo jeraha hupona haraka. Kuku wakubwa na wadogo wanaweza kutumia vyombo hivi, lakini mfugaji inambidi kukata kuku midomo kati ya majuma matatu hadi tano. Mdomo unaokatwa ni wa juu, na ukatwe kuanzia robo hadi nusu ya mdomo. Majogoo ya kupandisha yasikatwe kwa sababu yatashindwa kupanda.

Source:mitandaoni.

No comments:
Andika comments

Shukrani

Aina za Habari

Hifadhi