Thursday, May 12, 2016

Kanisa la CCF lagoma kuhama

Familia inapokaa pamoja
KANISA la City Christian Fellowship(CCF) lililopo Sinza Palestina lililoamuliwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kuhama mara moja tangu Aprili 28 mwaka huu halijatii amri hiyo ya mahakama.

Mtanzania ilipata hukumu ya mahakama hiyo ikionyesha kwamba mlalamikaji katika kesi ya madai namba 237 ya mwaka 2004, Prosper Rweyendera alishinda kesi na kutambulika kwamba ni mmiliki halali wa eneo hilo la kanisa .

Hukumu ya Mahakama iliyotolewa na Jaji John Mgetta aliyesikiliza kesi hiyo iliyofunguliwa dhidi ya Godfrey Mallasy na wenzake wakibishania umiliki wa jengo hilo la kanisa.

Ilidaiwa kuwa kanisa lilikuwa limepanga katika jengo hilo kwa makubaliano ya kulipa kodi lakini baadaye walionyesha kwamba walinunua na walikuwa wameshalipa malipo ya awali Sh milioni 20.

Ubishani huo ulifanya mlalamikaji kufungua kesi ambapo mahakama imebariki kwamba ndiye mmiliki halali wa eneo hilo plot namba 932 Block C, kiwanja namba 32759.

Mahakama hiyo iliamuru kanisa kukabidhi jengo hilo kwa mlalamikaji, kulipa kodi ya Sh milioni moja kila mwezi kuanzia Novemba 2004 hadi sasa na kulipa gharama zote za kesi.

Akijibu kwanini kanisa halijaondolewa pamoja na kutolewa kwa hukumu hiyo, Mchungaji wa Godfrey Imalassy alisema wameshindwa kutekeleza agizo la mahakama kwa sababu ya kutoridhika na uamuzi.

Mchungaji Imalassy alisema tayari wameshakata rufaa mahakamani hapo kupinga hukumu hiyo iliyolitaka kanisa kuhama mara moja.

“Baada ya mahakama kuamuru sisi tuhame na tuvunje kanisa,tuliona kuwa hatuwezi kuvunja kwa sababu hatujapata haki yetu kisheria ndipo tulipoamua kukata rufaa kwa ajili ya usikilizwaji mpya wa kesi,”alisema Imalassy.

Awali hukumu hiyo iliyosomwa na Msajili wa Mahakama, Jaji Richard Kabate kwa niaba ya Jaji Mgetta ilisema mahakama imejiridhisha na ushahindi uliotolewa na pande zote mbili, imekubaliana na hoja za upande wa walalamikaji uliowakilishwa na Wakili Joseph Rutabingwa kwamba umesinda kesi hiyo.

No comments:
Andika comments

Shukrani

Aina za Habari

Hifadhi