Ndiyo! kilimo ni Bishara, lakini kilimo ni Sayansi, kilimo ni utamaduni,kilimo ni Afya, Kilimo ni Elimu, kilimo ni Uchumi wa Nchi nyingi duniani. Hapa tutakupitisha kila kipengele cha kukufanya uwe mkulima stadi mwenye kufaidika na kazi yako ya kilimo wakati huo huo kwa wafugaji kadhalika mtafaidika na Blog hii ambayo imedhamiria kukueleza moja kwa moja kutoka kwa mkulima mwenyewe. Mkulima mwenye uzoefu ambaye atakutia nguvu kwa jinsi atakavyokupitisha katika changamoto alizokutana nazo.
Ili uweze kushika muhimili huu mkuu wa uchumi hapa nchini, kama mkulima zipo hatua muhimu ambazo unapaswa kuzipitia ama kuzitekeleza.
PIMA UDONGO
Hatua ya kwanza mkulima anatakiwa apime udongo wake kwa kutumia wataalam wa kilimo. Kupima udongo ni hatua ya kwanza katika zao lolote ambalo mkulima anakusudia kupanda. Ni kanuni muhimu kwani ndio itakuwezesha kukupa mwongozo wa aina ya mazao uyapandayo, utumie mbolea gani na usitumie mbolea gani katika shamba lako.
PIMA KIWANGO CHA MVUA
Hatua ya pili ni kupima kiwango cha mvua katika eneo la shamba lako. Hii ni hatua muhimu ambayo itakufanya ujue kupangilia mazao gani hasa upande kwa msimu husika. Mkulima anapaswa ajue kwa uhakika hali halisi ya mvua kama atalima kwa kutegemea mvua au maji ya mito ya msimu.
CHAGUA MBEGU BORA
Hatua ya tatu ni kuchagua mbegu bora. Ili upate mavuno ya uhakika unapaswa upate mbegu bora. Mbegu bora ni zile zilizoboreshwa kitaalam na kufanyiwa utafiti wa kina kuhusu uzaaji wake na faida zake katika mmea utokao hapo. Mbegu hizi utazipata katika maduka maalum ya pembejeo za Kilimo.
JUA SOKO
Hatua ya nne ni kujua soko la kila zao unatamani kulima. Soko ni kiungo muhimu katika zao lako kwa sababu hutafanya kilimo cha kubahatisha. Itakusaidia kufanya makadirio vizuri ya gharama za shamba, mazao hadi kuvuna.
MJUE MSHINDANI WAKO
Hatua ya tano ujue nani unashindana naye katika hayo mazao. Jua nguvu yake ya kiuchumi. Jua maarifa yake katika zao mnalolima wote. Angalia kama unaweza kushirikiana naye au ukishindwa nenda kajifunze kutoka katika maarifa yake.
UBORA WA BIDHAA ZAKO ZIKUTAMBULISHE SOKONI
Hatua ya sita ni kujijengea jina kwa ubora wa bidhaa zako.Hakikisha mazao yako yanakidhi wiango vyote vya ubora vinavyohitajika sokoni hasa kwa mlaji. Hakikisha hutumii dawa za kuulia wadudu ambazo ni sumu kwa mlaji. Hakikisha unawatumia wataalam washauri wa kilimo watakao kushauri vizuri na kwa njia sahihi.
HAKIKISHA HUPOTEI SOKONI
Hatua ya saba ni kujijengea uwezo wa kubaki sokoni. Hakikisha kuwa kila msimu upo sokoni ili usipoteze wateja. Kidhi mahitaji ya soko kila wakati.
No comments:
Andika commentsShukrani