Tangazo

Monday, January 9, 2017

HATUA SABA KATIKA KILIMO BIASHARA

Ndiyo! kilimo ni  Bishara, lakini kilimo ni Sayansi, kilimo ni utamaduni,kilimo ni Afya, Kilimo ni Elimu,  kilimo ni Uchumi wa Nchi nyingi duniani. Hapa tutakupitisha kila kipengele cha kukufanya uwe mkulima stadi mwenye kufaidika na kazi yako ya kilimo wakati huo huo kwa wafugaji kadhalika mtafaidika na Blog hii ambayo imedhamiria kukueleza moja kwa moja kutoka kwa mkulima mwenyewe. Mkulima mwenye uzoefu ambaye atakutia nguvu kwa jinsi atakavyokupitisha katika changamoto alizokutana nazo.

Ili uweze kushika muhimili huu mkuu wa uchumi hapa nchini, kama mkulima zipo hatua muhimu ambazo unapaswa kuzipitia ama kuzitekeleza.

PIMA UDONGO

Hatua ya kwanza mkulima anatakiwa apime udongo wake kwa kutumia wataalam wa kilimo. Kupima udongo ni hatua ya kwanza katika zao lolote ambalo mkulima anakusudia kupanda. Ni kanuni muhimu kwani ndio itakuwezesha kukupa mwongozo wa aina ya mazao uyapandayo, utumie mbolea gani na usitumie mbolea gani katika shamba lako.

PIMA KIWANGO CHA MVUA

Hatua ya pili ni kupima kiwango cha mvua katika eneo la shamba lako. Hii ni hatua muhimu ambayo itakufanya ujue kupangilia mazao gani hasa upande kwa msimu husika. Mkulima anapaswa ajue kwa uhakika hali halisi ya mvua kama atalima kwa kutegemea mvua au maji ya mito ya msimu.

 

CHAGUA MBEGU BORA

Hatua ya tatu ni kuchagua mbegu bora. Ili upate mavuno ya uhakika unapaswa upate mbegu bora. Mbegu bora ni zile zilizoboreshwa kitaalam na kufanyiwa utafiti wa kina kuhusu uzaaji wake na faida zake katika mmea utokao hapo. Mbegu hizi utazipata katika maduka maalum ya pembejeo za Kilimo.  

JUA SOKO

Hatua ya nne ni kujua soko la kila zao unatamani kulima. Soko ni kiungo muhimu katika zao lako kwa sababu hutafanya kilimo cha kubahatisha. Itakusaidia kufanya makadirio vizuri ya gharama za shamba, mazao hadi kuvuna.

MJUE MSHINDANI WAKO
Hatua ya tano ujue nani unashindana naye katika hayo mazao. Jua nguvu yake ya kiuchumi. Jua maarifa yake katika zao mnalolima wote. Angalia kama unaweza kushirikiana naye au ukishindwa nenda kajifunze kutoka katika maarifa yake.

UBORA WA BIDHAA ZAKO ZIKUTAMBULISHE SOKONI

Hatua ya sita ni kujijengea jina kwa ubora wa bidhaa zako.Hakikisha mazao yako yanakidhi wiango vyote vya ubora vinavyohitajika sokoni hasa kwa mlaji. Hakikisha hutumii dawa za kuulia wadudu ambazo ni sumu kwa mlaji. Hakikisha unawatumia wataalam washauri wa kilimo watakao kushauri vizuri na kwa njia sahihi.  

HAKIKISHA HUPOTEI SOKONI
Hatua ya saba ni kujijengea uwezo wa kubaki sokoni. Hakikisha kuwa kila msimu upo sokoni ili usipoteze wateja. Kidhi mahitaji ya soko kila wakati.

Monday, August 22, 2016

Wafahamu Ng'ombe wa Nyama, Bonsmara





Je, wewe ni Mfugaji?  Je, unafuga ng'ombe wa Nyama? Je unawajua Bonsmara? leo Sitawi inakustawisha na Kitu kizuri kitu cha Ukweli Sokoni. Ukitaka kufanya bisahara nzuri ya Nyama, fuga Bonsmara.

Bonsmara

Ni ng'ombe pekee duniani aliyeboreshwa na kurekodiwa vema tangu mwanzao hadi mwisho. Bonsmara ni ng'ombe aliyetokana na utafiti uliofanywa na Professa Jan Bonsma miaka ya 1964, huko Afrika ya Kusini. 
Ng'ombe huyu ni mchanganyiko wa 5/8 Afrikaner, 3/16 Hereford na 3/16 Shorthorn animals.

Jina la ng'ombe huyu lilitokana na kuunganishwa kwa majina mawili moja likiwa la Professa Bonsma na la pili ni Mara ambako ndiko utafiti ulikofanyikia. hivyo kupatikana kwa jina la Bonsmara.

Ng'ombe yeyote anafanya vizuri akiwa katika mazingira mazuri. Kiangazi, ukuaji na uzaaji unaweza kumfanya Ng'ombe asifanye vizuri. kwa mazingira yetu ya Afrika ambako kuna magonjwa mengi ya mifugo, wadudu kama kupe ni adui mkubwa kwa mfugaji. Huyu Bonsmara alizalishwa kuweza kuzishinda hizo hali ngumu za magonjwa na hali ya hewa. 
Ndama na mamake Bonsmara 
Bonsmara anakuwa haraka na ana uzito mkubwa kuliko ng'ombe wowote wale wa nyama Barani Afrika.

Stawisha Nywele kwa Beetroot

 

Je, unatatizo la kukatika Nywele?

Je,umewahi kujiuliza kwa nini ukichana nywele zinabaki rundo kwenye kitana? kwa nini ukichana nywele zako zinapukutika na kudondondoka? Je wajua vile ulavyo ni muhimu zaidi?

Kukatika kwa nywele ni tatizo kwa watu wengi. Wengi wao pia huwa hawajui wafanye nini ili kurejesha uoto wa asili katika nywele zao. Sababu zipo nyingi na  kubwa huwenda ikawa ni kukosekana kwa virutubisho muhimu mwilini au msongo wa mawazo.

Sitawi leo inakuletea namna bora kabisa ya kustawisha nywele zako kwa kutumia Beetroot. Beatroot ni maarufu kwa kuongeza damu mwilini kutokana na kuwa na uwingi wa madini chuma. Lakini leo Beatroot inakuongezea virutubisho ambavyo vitazuia nywele zako kukatika au kunyonyoka.

Beetroot ina vitamini C, madini ya Chuma, Vitamini B6, Magnesium na Potassium. Beetroot huondoa kabisa ukavu katika ngozi ya kichwa na hivyo kuzuia nywele kukatika. Kutokana na kuwa na virutubisho murua hivyo huifanya ngozi yako ya kichwa kuwa nyevu na yenye afya.

Sharubati (juice) ya beetroot pia ni nzuri kupunguza msongo wa mawazo. Kwa hiyo basi kama unakatika nywele kwa kuwa unamsongo wa mawazo basi Beetroot ni suluhisho lako.

Beetroot
Jinsi ya kutumia
Zipo njia nyingi za kutumia beetroot kustawisha nywele.

Unaweza kula katika salad, au kunywa kama Sharubati. Sharubati ya Beetroot inawasidia watu wengi sana wenye tatizo la kukatika ama kunynonyoka nywele.
lakini pia unaweza kuchanganya Lettuce na Beetroot au ukachanganya Beetroot na karoti.  Spinach na karoti pia ni nzuri sana katika kustawisha nywele.
Kula kama Salad, osha vizuri ondoa ganda la juu katakata vizuri vipande vidogo vidogo unaweza kuongeza veneger au unaweza kuongeza kajichumvi kidogo na pilipili manga au ladha yoyote uipendayo.

Salad ya Beetroot na Karoti


Njia nyingine nzuri unaweza kusaga kisha ukapakaa katika ngozi ya kichwa chako. Pakaa uiache ikae kwa muda wa dakika 15 hadi 20. Hii inasaidia kuuondoa vizuizi vya kustawi kwa nywele zako hasa mba. Mba ni adui mkubwa wa nywele. 
Hivyo basi Beetroot ni kirutubisho asilia kabisa cha kuotesha nywele zinazokatika. Kukatika kwa nywele ni ishara kwamba unakosa virutubisho muhimu mwilini mwako. Vyakula asilia ni muhimu sana na vinasaidia kuzuia nywele kukatika hovyo. 
Tukutane hapa wakati mwingine.

Sunday, August 14, 2016

Vijimambo vya Ujauzito


Mambo Haya huwezi kuelezwa na daktari

Kipindi cha ujauzito kimejaa mambo mengi ya kustaajabisha. Lakini kwa akina mama watarajiwa kwa mara ya kwanza hujumuisha mambo ambayo hakuyatajaria kuwa ni ya kawaida katika kipindi hicho. Mambo haya pia si rahisi kuambiwa na daktari yeyote. Ila ni muhimu uyajue.

Kuwashwa tumboni
"Katika mwezi wa saba wa ujauzito wangu, nilipatwa na muwasho tumboni kiasi kwamba nilikuwa siwezi kuvumilia” anakumbuka Skola John

Wataalam wa afya ya uzazi na magonjwa ya akina mama wanasema kuwa hali hii inasababishwa na ukavu wa ngozi na kutanuka kwa ngozi kutokana na kukua kwa mtoto. Hivyo inashauriwa endapo utakutwa na hali hii usijikune sana kwani inaweza kusababisha upate alama za mikwaruzo  badala yake jitahidi kujipaka mafuta ya kuainisha ngozi mara kwa mara. Pendelea kupaka Mafuta ya nazi au olive oil.



Hata hivyo kipindi cha ujauzito akina mama wengi pia husumbuliwa na matatizo mbalimbali ya ngozi.Ni muhimu kuwa mwangalifu pindi uonapo dalili ambazo sio nzuri katika ngozi yako ukamuona daktari ambaye ni mtaalam wa mausala yanayohusu ngozi au uendepo kliniki muulize daktari wako akupe mwongozo mzuri wa uhakika.

Monday, August 8, 2016

Ubora wa Maziwa ni kwa kula mlo Kamili .

Kwa mama unayenyonyesha tambua kuwa maziwa anayopata mtoto kutoka  kwako ubora wake hutokana na kile chakula ulichokula ukiwa mjamzito na hadi sasa unaponyonyesha.
Inashauriwa kwa mama anayonyesha kula mlo kamili ili mtoto apate virutubisho vyote muhimu vitakavyojenga afya ya mwili na ya akili na ukuaji kwa ujumla.  

Baadhi ya akina mama huwa wanashindwa kutofautisha kati ya vichocheo vya kuongeza maziwa na ubora wa maziwa. Mfano mama anayejifungua kwa mara ya kwanza huweza kujikuta hatoki maziwa. Kwa kawaida watu walio karibu naye humshauri anywe uji wa pilipili na supu kwa wingi, nyanya chungu,kutafuna mihogo na vingine vingi. Wakati mwingine anaambiwa anywe chai ya tangawizi. Lakini ikumbukwe kuwa huu  sio mlo wa mama anayenyonyesha. Bali ni vichocheo vya kuchagiza maziwa yatoke. Kimsingi kutotoka kwa maziwa kunasababishwa na mmabo mengi ikiwemo kutokuwa tayari kwa mzazi kisaikolojia. kutokuwa tayari kunahusisha hofu au uoga wakati mwingine hekaheka za kipindi cha ujauziti zilimchosha mama, lakini kubwa kuliko yote ni mlo gani alikuwa anakula mama huyo kipindi akiwa mjamzito?
Ubora wa viini lishe vinapatikana katika chakula ambacho kimezingatia Makundi yote  ya chakula.Supu ya mboga mboga ni muhimu sana  kwa ajili ya vitamini. 
Mlo  uliokamilisha makundi yote ya chakula. 

(Picha hii ni kwa hisani ya #wives_and_mothers)
Mama anayekula vizuri maziwa huwa mengi na yenye Ubora. 

Sunday, August 7, 2016

NaneNane Morogoro,Ufugaji Samaki katika Matank

Ikiwa kesho ndio kilele cha NaneNane usikose kuja kuona fursa zikufaazo.
Kwa mkulima makini na unayetaka kujikita katika kilimo cha biashara usikose kufika Banda la Chuo kikuu cha kilimo  Sokoine ujionee utaalam Mpya wa ufugaji Samaki katika Matanki.

Tanki  hili limetengenezwa kitaalam na linauwezo wa kukuzia Samaki sawasawa na walio katika mabwawa. Faida moja Wapo na ya kipekee tanki ni nafuu kuliko mabwawa ya kuchimba na samaki hutumia muda wa miezi minne  hadi kuvunwa. Faida nyingine ni kutumia eneo dogo  zaidi kulinganisha na mabwawa ya kuchimba. 
Tembelea Banda la SUA kwa maelezo zaidi. 

Saturday, August 6, 2016

Waziri wa Afya Ataka TFDA kuchunguza Mayai

Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mayai ya kuku wa kisasa yanayotengenezwa nchini  yamedaiwa kuwa na mabaki ya dawa ambazo ni hatari kwa  afya ya binadamu.

Akizungumza leo wakati alipozindua bodi  mpya ya ushauri ya wizara kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA), Mwalimu amesema amehakikishiwa na wataalamu hao kuwa dawa zinazotumika kwenye mayai na kuku hao zinabaki ambapo si salama kwa afya ya binadamu.

Mwalimu amesema kutokana na dawa hizo kubaki kwenye mayai na kuku hao ameitaka TFDA kufanya utafiti  ili kujua  kiwango kipi cha dawa zilizopo ili  Serikali iweze kuchukua hatua za  haraka. 


"Hivyo tuwaachie TFDA waendelee na utafiti wao na wanapobaini ni kiasi gani cha dawa zilizomo kwenye mayai na kuku hao watuambie haraka dawa zipi hazitakiwi na zipi zinatakiwa ili kulinda soko la ndani,”alisema.

Pia amewatahadhalisha wataalamu wa TFDA wasihofie kutoa majibu haraka kwa kufikiri kuwa watakwamisha soko la ndani hivyo wanatakiwa wawe wa kweli ili tatizo lililopo liweze kupunguzwa.
Usikose lutembelea hapa kuhusu ufugaji bora wa kuku usio na madhara
Mhe. Waziri Ummy Mwalimu. 

Tuesday, August 2, 2016

Serikali ya Tanzania kukata Rufaa Ndoa za Utotoni


Serikali ya Tanzania imewasilisha ombi la kukata rufaa, uamuzi wa kihistoria nchini uliopinga ndoa za watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

Mwezi uliopita mahakama kuu iliamua kuwa sehemu za sheria ya ndoa mwaka 1971, iliyoruhusu wasichana kuolewa wakiwa na umri wa hata miaka 14 ni kinyume na katiba.

Kundi la kutetea haki za watoto "Msichana Initiative" iliwasilisha kesi hiyo mahakamani. Taarifa hiyo ya kukata rufaa imewashtusha wengi Tanzania , wengi wakishindwa kuelewa ni kwanini mkuu wa sheria angetaka kugeuza hukumu hiyo.

Mwezi uliopita mahakama kuu iliipa serikali muda wa mwaka mmoja kurekebisha kosa hilo na kuweka umri wa miaka 18 kama umri sahihi wa watu kufunga ndoa, kwa wote wasichana na wavulana nchini.

Awali sheria ya ndoa ya mwaka 1971 nchini Tanzania imetaja kuwa wavulana wanapaswa kuoa wakiwana miaka 18 huku wasichana wakiwa na umri wa miaka 15. Kesi hiyo iliwasilishwa na kundi la kutetea haki za watoto Msichana Initiative, kupitia wakili Jebra Kambole.
Asilimia 37 ya wasichana walio na umri wa chini huolewa Tanzania.

Wasichana wenye umri wa hata miaka 14 huozwa kwa idhini ya wazazi. Na wengi wao baadaye huripotiwa kukabiliwa na unyanyasaji nyumbani na hutengwa katika jamii - wakikosa nafasi za kusoma na kuajiriwa.
Hivi karibuni bunge lilikarabati kipengee cha sheria ya elimu na sasa ina sehemu inayotoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 gerezani au faini ya dola 2500 kwa wanaume wanaowapachika mimba au kuwaoa wasichana wa shule.

Chanzo:BBC, Swahili

Wiki ya Unyonyeshaji Duniani

Nchi zaidi ya nchi 170 duniani zinasherehekea wiki ya unyonyeshaji kuanzia Agosti Mosi hadi Agost 7, ili kuchagiza jukumu la onyonyeshaji kwa lengo la kuboresha afya wa watoto kote duniani.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO kunyonyesha ni njia bora ya kuwapatia watoto wachanga virutubisho muhimu na vya kipekee wanavyohitaji mwilini.

Shirika hilo linapendekeza watoto kupewa maziwa ya mama mara tu anapozaliwa kuanzia saa moja baada ya mtoto kuzaliwa hadi miezi sita.

(Picha kwa hisani ya peacefulearthgracefulbirth.worldpress. com). 
Maziwa ya mama ndio chakula pekee cha mtoto wa kuanzia mwezi sifuri hadi sita kinachomjenga mtoto kimwili, kiakili na kijamii.  
Kunyonyesha sio tendo tu la kumpa mtoto chakula chake bali ni  moja Wapo ya sehemu ya Malezi ya mwanzo. 
Kila  mama anayenyonyesha hufanya mahusiano ya kijamii na mwanae. Mtoto anaponyonya anajifunza upendo kutoka kwa mama ndio maana akinyonya huwa haachi kumwangalia mama yake usoni ili aisome ishara. kadiri anavyoendelea kunyonya mtoto huanza pia kutaka kujaribu mamlaka ya mama kwake. Na hapa mama anapaswa kujua hilo jaribio likichekewa mtoto anakudharau. Ukiwa unamnyonyesha mtoto akakuuma ujue huo sio mchezo. Mkemee haraka sana.Na hatarudia. Kuna maelezo mengi kuhusu hiyo tabia lakini usimng'ate na wewe au kumchapa kibao au chocolate cha kuumiza mwili bali akikuuma mnyime kunyonya kwa wakati huo kisha mpe  aendelee akirudia tena mnyime hadi aelewe titi ni la kunyonya tu sio kuuma. 
Ukifanya hivyo utakuwa umeweka msingi wa kwanza wa kutii mamlaka. 

Hata hivyo kwa Mujibu wa Utafiti uliofanywa na wizara ya afya nchini imebainika kuwa ni asilimia 51% tu ya watoto wenye umri wa Miezi 0 hadi sita  wanaonyenyeshwa kikamilifu. 
Inashauriwa
 Mtoto anyonye hadi umri wa miaka mwili. 
#chochea tabianjema@mnyonyeshemtoto kwa maendeleo
tukutane kesho. 

Monday, August 1, 2016

NaneNane, 2016

Mahindi ya Njano. 

Ujio wa mbegu hii ya Njano umeleta mapinduzi katika Tija  ya Mkulima wa Mahindi nchini. Mkulima Sasa anauwezo wa kupata gunia zisizopungua 20 katika ekari moja. 

Mbegu hii ni hybrid. C. P201. 
Mbegu hii pia imeboresha Afya ya mlaji. Ni  Mahindi ya Njano pekee yenye virutubisho vya carotene ambavyo havipo kwenye mahindi meupe. Kwa hiyo basi ulaji wa Mahindi ya Njano yanakuongezea hiyo carotene ambayo ni shabili na Vitamin A na C ambazo katika vyakula vitokanavyo  na nafaka utavipata katika mahindi haya ya Njano pekee. 
Tembelea leo Maonyesho ya Nane Nane Morogoro na ufike katika band's  la kampuni ya CPP. 

Aina za Habari

Hifadhi