Friday, April 29, 2016

H’mashauri zabanwa mfumo wa elektroniki

Mfano wa logo ya Sitawi
SERIKALI imesema ifikapo Julai Mosi, mwaka huu halmashauri zote nchini ziwe zimefunga na kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato yake ya ndani na kusitisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mawakala.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti yake bungeni juzi jioni.

Pamoja na mambo mengine, Simbachawene alisema kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki katika maeneo mbalimbali ya serikali, kuanzia Julai Mosi mwaka huu halmashauri zote nchini ziwe zimefunga na kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato yake ya ndani.

“Naziagiza halmashauri kwamba, mara baada ya mikataba ya sasa kwisha, ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mawakala usitishwe badala yake makusanyo yafanywe na maofisa wa halmashauri kwa kutumia mifumo ya kielektroniki,” alisema Simbachawene.

Alisema katika mwaka wa fedha unaomalizika, watumishi 78 wa mamlaka za serikali za mitaa walichukuliwa hatua za kinidhamu na kijinai.

“Kati ya watumishi hao, wakurugenzi wa halmashauri watano wamevuliwa madaraka na kupangiwa kazi nyingine na wakurugenzi watatu wamefunguliwa kesi mahakamani na kesi hizo bado zinaendelea.

“Watumishi wengine ni wakuu wa idara na watumishi wa kawaida  wa halmashauri ambao wapo waliofukuzwa kazi, kuachishwa kazi na wengine kushitakiwa mahakamani.

“Hadi kufikia Machi mwaka huu, watumishi 90 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na wengine kufikishwa mahakamani,”alisema Simbachawene.

Alisema kati ya watumishi hao, wakurugenzi watatu wamevuliwa madaraka na kupangiwa kazi nyingine, watano wamefikishwa mahakamani, kumi wamesimamishwa kazi na kupewa mashitaka  ya  nidhamu.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki akiwasilisha hotuba ya ofisi hiyo alisema kuanzia sasa viongozi wa Serikali wakiwemo wa ngazi za juu watakaobainika kuhusika kwa njia yoyote katika kufanikisha ulipaji wa mishahara hewa watafunguliwa kesi za jinai.

“Uchumi imara na endelevu katika nchi yoyote unahitaji uwepo wa utumishi wa umma uliotukuka unaozingatia utawala bora, utawala wa sheria, maadili na mifumo thabiti ya usimamizi na utekelezaji.

“Mipango na bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa ofisi ya rais  imezingatia dhamana hiyo ambayo imebeba dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kuleta mabadiliko makubwa katika utumishi wa umma kwa kuimarisha uwajibikaji na uadilifu,”alisema waziri huyo.

Alisema utekelezaji wa dhamira hiyo utasaidia kujenga utumishi wa umma uliotukuka kwa kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka.

“Ni lazima tuwe na viongozi wa umma wanaozingatia maadili yao ya kazi na ndio maana tunasisitiza kuwa viongozi wote watakaobainika kuhusika na ulipaji au kusaidia kulipa watumishi hewa mishahara, tutawafungulia kesi za jinai,” alisema Kairuki.

No comments:
Andika comments

Shukrani

Aina za Habari

Hifadhi